- Mifugo
Sambaza chapisho hili

Umuhimu wa kuotesha malisho kukabili ukame

Malisho yaliyo mengi hapa nchini ya asili ambayo hutegemewa na mifugo hukomaa na kukauka mapema zaidi na hivyo kusababisha lishe kwa wanyama kuwa duni wakati wa kiangazi ambapo wanyama huhangaika sana kupata chakula.

Kutokana na upungufu huo ni vyema wafugaji kuotesha aina mbalimbali za malisho bora ili kunusuru mifugo yao wakati wa ukosefu wa chakula katika malisho ya asili.

Mfugaji anatakiwa kutayarisha eneo la shamba ambalo atalitumia kuotesha malisho yake, pamoja na kurutubisha eneo hilo.

Namna ya kutayarisha shamba

Kabla ya kulima eneo la shamba unalokusudia kuoteshea malisho, ni vyema ukaweka mbolea ya mboji au samadi iliyoiva vizuri ili kurutubisha udongo na kufanya kupatikana kwa malisho yenye ubora na mengi.

Eneo la kuoteshea malisho linatakiwa lisafishwe vizuri kwa kuondoa vichaka pamoja na miti kukata ambayo yatazuia ulimaji wa eneo kufanyika vizuri.

Baada ya kusafisha shamba lilimwe kwa kutumia jembe la mkono, plau ya ng’ombe au aina yoyote ya ulimaji. Hakikisha shamba limelimwa vizuri na udongo umetifuliwa vizuri ili kuwezesha mbegu kutoka mapema bila kizuizi.

Mbegu

Chagua mbegu bora inayoaminika kufanya vizuri katika uzalishaji wa malisho.

Ni vyema kununua mbegu za kupanda kutoka katika mashamba yanayoaminika kuwa na ubora na yasiyo na magonjwa wala wadudu.

Upandaji

Ni vyema kupanda mbegu wakati wa mvua ili kusaidia uotaji na ustawi mzuri wa mbegu.

Kama mbegu ni ya kusia, chora mistari kisha weka mbegu katika mistari hiyo. Wakati wa kusia, ni vyema ukachanganya mbegu na mchanga kuzuia mrundikano wa mbegu nyingi sehemu moja. Baada ya kusia mbegu tumia tawi la mti kuburuza shambani ili kufunika mbegu.

Ikiwa utatumia mapandikizi, ni vyema ukachagua vishina vidogo vyenye afya kisha kuviotesha kwenye mistari na katika mashimo ambayo umekwisha kuyaandaa.

Palizi

Ikiwa magugu yameota mapema, ni vyema ukaondoa ili kufanya malizho kuota na kustawi .vizuri

Urutubishaji wa malisho

Pale unapoanza kutumia malisho, ni vyema kuendelea kuweka mbolea ya samadi ili kuendeleaa kurutubisha udongo na kuendelea kuzalisha malisho mengine mengi zaidi kuliko yale ya mwanzo na yenye ubora.

Kuchungia malisho

Ikiwa malisho ya kuvuna, mfugaji anatakiwa kuchunga mifugo kwa utaratibu mzuri ambao hautafanya uharibifu wa malisho. Ni vizuri pia kutumia eneo moja baada ya jingine na si kuchunga mifugo katika eneo lote.

Kuvuna malisho

Malisho yanaweza kuvunwa na kuhifadhiwa wakati ambapo malisho ya asili yanatumika hivyo kulishia mifugo katika kipindi cha kiangazi ambapo malisho ya asili yatakuwa yameisha.

Baada ya kuvuna, yahifadhiwe katika stoo iliyoandaliwa na isiyokuwa na unyevu wala kuruhusu mvua.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *