Ugonjwa wa miguu na midomo (FMD)

Huu ni ugonjwa unaowashika ng’ombe, kondoo, mbuzi, pamoja na wanyama wa porini kama mbogo, swala na wakati mwingine tembo. Ng’ombe anapopatwa na ugonjwa wa miguu na midomo huchechemea na asipotibiwa kwa haraka hushindwa kusimama na kula hatimae hudhoofika na hata kufa.

Ugonjwa wa miguu na midomo husambaa haraka kwenye kundi ukiua ndama na kusababisha wanyama kupoteza uzito na uzalishaji wa wengine kupungua.

Namna unavyoambukizwa

Ugonjwa huu unaambukiza kwa kugusana kwa mnyama mmoja na mwingine. Unaweza vile vile kusambazwa na upepo kwenye umbali hata wa kilometa 250. Pamoja na kusambaa kwa umbali huo, ni nadra kwa binadamu kupata ugonjwa huu.

Kwa muongo mmoja uliopita, wastani ugonjwa huu ulikuwa unashambulia kundi mara moja kwa mwaka. Kwa sasa, katika sehemu nyingi za Afrika Mashariki, ugonjwa unatokea mara tatu kwa mwaka. Aidha, jinsi hali ya hewa inavyokuwa ya joto la juu, yanatokea matabaka mapya ya vimelea visababishavyo ugonjwa huu.

Dalili

• Kuwepo mifugo yenye dalili za mafua, na kuchechemea kwa wakati huo huo.

• Ndama kufa kwa ghafla kutokana na ugonjwa wa moyo.

Tahadhari

Ugonjwa wa miguu na midomo una madhara makubwa kiuchumi hasa ukizingatia kuwa, uzalishaji wa maziwa wa ng’ombe waweza kupungua kwa asilimia 75 kwa maisha yake yote.

Mbali na hayo, ng’ombe badala ya kuzaa kila mwaka au kwa vipindi kama hivyo, anaweza kuzaa kila baada ya miaka miwili au mitatu.

Namna ya kuzuia

Chanjo kwa ajili ya ugonjwa huu husaidia kuzuia isipokuwa gharama yake ni kubwa kwani chanjo hizo zinanunuliwa kutoka nchi za nje na lazima iwe ya kufanyakazi dhidi ya aina nyingi za vimelea. Hata hivyo, jamii inaweza kupanga, na kununua chanjo kwa kushirikiana.

Ugonjwa wa miguu na midomo ni tishio, hasa katika maeneo ambapo mifugo inatumia ardhi ambayo pia inatumiwa na mbogo na nyumbu. Ni vyema kwa wale wanaoishi katika maeneo hayo kuhakikisha kuwa ardhi wanayotumia kulishia mifugo yao si ile inayotumiwa na wanyama pori.

Ugonjwa wa nyumbu (Malignant Catarrhal Fever -MCF)

Ugonjwa wa Nyumbu ni ugonjwa ambao husababishwa na virusi aina mbili kwa ng’ombe. Aina ya kwanza husambazwa na kondoo na mbuzi wakati aina nyingine husambazwa na nyumbu na pofu.

Aina ya pili ni tatizo kubwa hasa wakati na mahali ambapo nyumbu wanazalia. Virusi vinawaachia watoto wa nyumbu wanapotimiza miezi mitatu baada ya kuzaliwa.

Kwa karne nyingi, ugonjwa wa nyumbu ulikuwa hauwaletei wafugaji madhara makubwa kwa sababu walikuwa wanahamisha mifugo yao kwenda sehemu nyinginezo kila mwaka katika kipindi ambacho nyumbu wanazaliana.

Mpango huu wa kimila wa matumizi ya ardhi umesambaratika, ijapokuwa ni katika miongo michache iliyopita, kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya kutumia ardhi (mashindano) na hivyo ng’ombe na nyumbu kulazimika kupata malisho katika eneo moja hata katika vipindi nyeti ambapo nyumbu wanazaa. Bila kuchukua hatua za tahadhari, ng’ombe na nyumbu wataendelea kula katika eneo moja na hivyo uwezakano wa ugonjwa wa nyumbu kuongezeka pia ni mkubwa.

Dalili

Macho ya ng’ombe yanakosa uwezo wa kupitisha mwanga. Baada ya hapo mnyama anapofuka na kufa.

Kuzuia na kudhibiti

Hadi kufikia sasa, hakuna chanjo wala tiba ya ugonjwa huu isipokuwa suala la udhibiti unawezekana kwa kupitia matumizi mazuri ya ardhi. Mipango ya matumizi ya ardhi inabidi izingatie mahitaji ya wafugaji na uhamaji wa nyumbu na mazalia yao. Mipango inaweza kuweka eneo tofauti la malisho ya mifugo kwenye majira ya nyumbu kuzaa, ambayo kwa wastani yanaanza mwishoni mwa mwezi Februari hadi Mei.

Maelezo hayo ni kwa hisani ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO). Kwa maelezo zaidi, wasiliana na Francis Ndumbaro kwa simu +255 754 511 805.

Maoni

maoni yangu nahitaji kujua kwa undani kuhusu kilimo cha mbogamboga nahitaji sana. Naomba mnifahamishe kupitia email yangu

Habari

Ukisema mbogamboga zipo za aina nyingi sana, hivyo tunaomba useme ni aina ipi ya mbogamboga unahitaji kulima. Ni vigumu sana kukueleza aina zote za mboga kwa wakati mmoja kwani ni nyingi sana na ni nyingi pia ambazo tumeshazifanyia kazi.

Karibu sana mkulima mbunifu

Andika maoni mpya

Plain text

  • Hakuna vishikizo vya HTML vinavyokubaliwa
  • Anuani ya ukurasa kwenye mtandano na anwani za barua pepe hubadilika kuwa viungo moja kwa moja.
  • Mistari na aya zinajipanga zenyewe.